Etendeni Lami (Psalm 91) // WE WILL WORSHIP
Zaburi 91
1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
2 Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.
3 Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.
4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.
5 Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana,
6 Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,
7 Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.
8 Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.
9 Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.
10 Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.
11 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.